Ushawahi kujiuliza Ama kusikia mtu akisema, “ Mbona nimechanja na Kuku wangu bado wakaugua na Kufa!”
Ama Mganga/Daktari analaumiwa “Mbona Mbwa/paka wangu ameugua na Chanjo ulitoa?” Kabla ya kupata hayo majibu tujiulize kwanza CHANJO ni NINI?
Chanjo ni maandalizi ya kibailojia ambayo hutoa kingamwili(ulinzi) dhidi ya ugonjwa fulani, Kinga hiyo huwa ya Muda fulani au Maisha yote.
Chanjo kwa kawaida ni vijidudu(Antigen) hai ama mfu ambavyo vinavyosababisha ugonjwa huo ila huwa Vimefubaishwa ili kutokuleta madhara katika mwili na hutolewa katika kiwango ambacho huweza kuamsha kinga ya mwili dhidi ya ugonjwa husika.
Mfano. Chanjo ya Kideri (Newcasttle) ni Vijidudu hai vyenye kusababisha ugonjwa wa kideri lakini vilivyofubaishwa ili vitoe kinga kwa maambukizi yajayo ya Ugonjwa wa kideri/Mdondo.
Chanjo hufundisha mfumo wa kinga mwilini jinsi ya kutambua na kupigana na bakteria au virusi kabla ya maradhi kutokea.
Baadhi ya chanjo zinahitaji dozi moja tu Mfano Chanjo ya Ndui ilehali zingine zinahitaji dozi kadhaa ili kuandaa ulinzi kamili Mfano Chanjo ya Kideri/Mdondo
Ni vyema ikaeleweka kwamba SIO chanjo inayokinga mwili bali ni Mwili ndio hujikinga dhidi ya ugonjwa (Mwili ndio huzalisha kinga/Ulinzi). kuna Magonjwa ambayo mnyama au Ndege akiiugua na Akapona hawezi kuugua tena ugonjwa huo kwa sababu mwili unakua ushatengeneza kiwango cha kutosha cha ulinzi/Kinga dhidi ya huo ugonjwa Mfano NDUI kwa kuku, Surua kwa Binadamu.
Chanjo hutolewa kwa Njia zifuatazo
1. Njia ya hewa (Kuvuta)/Kupulizia.
chanjo iliyochanganywa na maji hupulizwa kwenye hewa na ndege huivuta kwa kutumia pua.
2. Kunywa/Maji/Maziwa yasiyo na Krimu.
Chanjo huchanganywa na Maji salama kisha ndege au wanyama hupewa na kunywa
Mfano. Kideri (Lasota strain)
3. Kuchoma/Sindano
Kwa kutumia Sindano maalumu Ndege huchomwa sehemu muhimu ama kwenye katika sehemu ya ngozi ya bawa au chini ya ngozi. Mfano Ndui na Gumboro.
4. Matone.
Chanjo hutolewa kwa njia ya matone ambayo hudondoshwa kwenye jicho
Mfano. Kideri.
SABABU ZA CHANJO KUSHINDWA KUMLINDA MNYAMA (KUFANYA KAZI).
1. Kushindwa kudhibiti hali ya joto ridi (4-8C).
Kwa kawaida chanjo hutunzwa katika Jotoridi (Ubaridi) wa Nyuzi joto 4-8 kulingana na Maelekezo ya Mtengenezaji.
Kwa hiyo basi Kuanzia kwa mpaka chanjo inapokufikia kabla ya kumpatia Ndege au Mnyama lazima iwe kwenye ubaridi huo wa 4-8C Katika hatua yeyote ile, Chanjo ambayo haikutunzwa katika Ubaridi huo basi ni fika Chanjo hiyo haitatoa kinga kwa wanyama wako na Ugonjwa ukija wataugua kama Wanyama wengine ambao hawakupata chanjo ya ugonjwa huo.
Kwa Hiyo kwa Chanjo bora na Imara ni lazima wadau wote, Watengenezaji, Wasambazaji na Wauzaji kuhakikisha Chanjo inatunzwa kwenye ubaridi unaotakiwa.
“Hii ndio sababu kuu kwa chanjo nyingi kushindwa kufanya kazi ipasavyo”.
NB: CHANJO HAITAKIWI KUGANDISHWA AU KUWEKWA KWENYE KIGANDISHIO(FREEZER)
2. Wanyama DHAIFU na WASIOPATA chakula sahihi au utaratibu Maalumu.
Udhaifu huu ambao husababishwa na Ugonjwa, Lishe mbaya (Isiyo bora) Husababisha mwili kushindwa kuzalisha kiwango stahili (cha kutosha) kukinga mwili dhidi ya ugonjwa husika ambayo Husababisha Ugonjwa pale Anaposhambuliwa na Wadudu.
Lakini pia kutokana na mwili kushindwa kuzalisha kiwango cha Kinga basi vimelea vile vinaweza kugeuka kua chanzo cha kulipuka kwa ugonjwa kwa mnyama au Shambani kwako.
NB: CHANJO HUTOLEWA KWA WANYAMA WENYE AFYA NJEMA NA WASIODHAIFU KWA HALI YEYOTE ILE.
3. Chanjo iliyokwisha Muda wake.
Hutokea mara chache sana ila ni vyema kuangalia muda wa kuisha matumizi ya chanjo (expire date) na kama haionekani vyema au Haipo ni vyema kutokununua hiyo chanjo au kutoitumia maana Vimelea vya chanjo hiyo havitakua na uwezo wa kuwa kinga wanyama wako.
4. Mwili kushindwa kutambua Viini vya chanjo (Vijidudu) na Kusababisha Kinga kutozalishwa(NON-RESPONDER).
Hii ni sababu ya Kibaiolojia na haisababishwi na ubora wa chanjo. Na Viumbe hawa huwa wachache sana kwenye kundi ila kwa Wanyama wanaomilikiwa wachache kama Mbwa, paka, Farasi nk huwa na Umuhimu sana.
Ni vyema kupima kiwango cha kinga (Antibody titter) baada ya kuchanja ili kujua kama Chanjo iliyotolewa imetoa kinga stahiki katika kundi lako la wanyama.
Wasiliana na Daktari wa Mifugo.
5. Kutumia Vichanganyishio au Njia isiyosahihi katika kutoa chanjo.
Kwa Mantiki hiyo Vichanganyishio (Maji/Maziwa yaliyoondolewa krimu(Skimmed milk) vinatakiwa Visiwe na Kamikali au sumu au Madini.
Kwa hiyo maji yeyote yanayotibiwa (Chlorinated), Maji ya Mvua (Kimikali na madini) na Ya visima (Viwango vikubwa vya madini), kemikali hizo Hupunguza ama kuua vimelea vya chanjo na kusababisha Ubora wa chanjo kupungua na wanyama wako kutolindwa kwa kiwango stahiki. (Zipo Viambata ambazo hazina madhara kwa viini vya chanjo na huchanganywa na maji kabla ya Kuweka chanjo ambazo hupunguza ama kuondoa madhara ya Chroline na Madini kwa vimelea vya chanjo).
USITUMIE MAJI YALIYOTIBIWA KUCHANGANYA NA CHANJO.
6. Toa chanjo wakati wa ASUBUHI ama JIONI kipindi joto la mazingira lipo chini.
Joto kali Husababisha hali ya Msongo(stress) kwa wanyama ama Ndege na kusababisha Taharuki kwa mwili wa mnyama ambapo inawezekana ikasababisha matokeo yasiyotarajiwa.
7. Matumizi ya dawa (Antibiotic) kabla au baada ya Chanjo.
Kama tulivyoona hapo mwanzo chanjo ni vimelea hai au umfu inamaana huathiriwa na dawa (antibiotics) kama wadudu wengine.
Ni vyema kutokutoa chanjo Siku 3 kabla ama kulingana na Muda wa kuisha mwilini wa dawa husika (Withdrawal piriod, kila dawa ina muda wake, tazama kwenye kibandiko cha dawa) kwa mantiki hiyo Chanjo itakua salamu kwenye mwili wa mnyama pia Siku 3 baada ya chanjo ili kuupa mwili Muda wa kutosha kuzalisha kinga.
8. Kiwango kidogo cha chanjo (dozi).
Hii hutokea pale unapotoa chanjo kidogo (vimelea vichache) ambayo hushindwa kuamsha Kinga ya mwili kwa kiwango cha kutosha ambapo Huletelezea mnyama kutopata kinga ya kutosha. Mfano Una Kuku 1600 unawapa chanjo yenye kutosha kuku 1000, maana yake Kuku ni wengi kuliko kiwango cha chanjo maana yake hawata pata kinga inayostahili kuwakinga na ugonjwa.
Mambo ya kuzingatia kabla ya kutoa chanjo.
1. Ni Vyema Chanjo itolewe katika Uangalizi wa Mganga(Dr) wa Mifugo.
2. Kabla ya kutoa chanjo Wasiliana na Mganga wa wanyama kuhakiki Afya wa wanyama wako (Usitoe chanjo kwa wanyama Dhaifu, Upungufu wa lishe ama wagonjwa).
3. Kama unatumia maji hakikisha Maji yako ni Salama kwa matumizi ya kuchanganyia Chanjo(Usitumie Maji yaliyotibiwa)
4. Toa Njanjo Asubuhi ama Jioni (Joto likiwa chini)
5. Usitumie dawa(Antibiotic) siku 3 kabla au baada.
6. Hakikisha chanjo yako haijaisha Muda wa matumizi.
Kwa Kufuata Utaratibu sahihi wa kutoa chanjo na Chanjo iliyobora, hakika Tutaepusha vifo vinavyotokana na Utoaji chanjo mbovu.
............................................................................................................
DOWNLOAD APP ZETU HAPA TOKA MSHINDO MEDIA
0 comments:
Post a Comment