KIDELI/MDONDO (NEW CASTLE DISEASE)
Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo huathiri mfumo wa upumuaji na neva za fahamu. Vifo vya vifaranga na kuku wakubwa huanzia asilimia 0 hadi 100%, itategemeana na kasi ya mashambulizi ya virusi hao.
Uzalishaji wa mayai hupungua kwa kasi kubwa hadi kufikia sifuri (0) ndani ya siku nne.
Kuku wanapalalaizi shingo na kupinda
Kuku wanakohoa na kupumua kwa shida na wakati mwingine hutokwa na majimaji puani.
Kuku wanaharisha muharo wa majimaji wenye rangi ya kijani mpauko.
Kuku wakianza kutaga tena, mayai yao huwa na sura isiyokua ya kawaida au sura iliyopindapinda.
Kuku wanakohoa na kupiga chafya
Kuku wanakaa wakiwa wamenyong'onyea viungo vya miguu na mara nyingine wanatembea kinyumenyume.
Kuku wanatembea kwa kuzunguka mduara au wanainamisha vichwa vyao katikati ya miguu.
Kuku wanakosa hamu ya kula, hali ikiwa mbaya sana wanakaa chini na kupoteza fahamu na baadae hufa.
Ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa, maji maji ya kuku kama udenda au kinyesi. Pia husambazwa kupitia vifaa mbalimbali vilivyochafuliwa na majimaji yaliyotoka kwa kuku kama udenda au kinyesi.
Pia Virusi vya kideli husambazwa kupitia mayai yaliyotagwa na kuku muathirika wa ugonjwa huu, Uzuri ni kwamba kiini cha yai lenye vimelea vya kideli hufa na yai kushindwa kuanguliwa.
Ugonjwa huu hauna tiba, bali hukingwa kwa chanjo.
Wapatie chanjo ya kideli kuku wako wenye umri wa wiki 3 hadi 4, pia rudia tena chanjo wakiwa na umri wa wiki 16 na wakifikia wiki 24. Baada ya hapo uwapatie tena chanjo mara uonapo kuna mlipuko wa ugonjwa kwenye eneo lako.
HOMA YA MATUMBO (FOWL TYPHOID)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vinavyoitwa gallinarum au shigella gallinarum. Dalili za ugonjwa huonekana siku 3 hadi 4 baada kuku kuingiliwa na vimelea, pia vifo huonekana ndani ya wiki 2 tangu kuona dalili. Ugonjwa huu husambazwa kupitia kuku walioathilika, vifaa mbalimbali ikiwemo vya kuku, viatu, unyevu unyevu ndani ya banda (hususani kwenye sakafu ya banda kama mapumba ya mpunga au malanda ya mbao), n.k
Kuku wanazubaa na manyoya yao yanakua hovyo hovyo tofauti na kuku wasiougua.
Kichwa chake hupauka, na upanga wa kichwani hulegea na kulala
Wanakosa hamu ya kula
Wanaharisha kinyesi cha rangi ya chungwa
Wape chanjo ya ugonjwa huu kwa kuku wenye umri wa wiki saba (7)
Teketeza kuku wote waliokufa kwa kuchoma moto
Usiruhusu watu mbali mbali kutembelea mazingira ya banda lako bila kuondosha vimelea (Disinfection) kwa kukanyaga sehemu yenye maji ya dawa (Footbath) kila wanapoingia au wanapotoka bandani.
Tumia dawa za oxytetracycline kama Furamax,Typhoprim hutibu ugonjwa huu.
PULLURUM DISEASE (MUHARO MWEUPE)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vinavyoitwa Salmonella Pullurum, vimelea hivi huathiri mfuko wa mayai wa kuku jike (Ovary). Vimelea hivi pia hukaa kwenye utumbo mwembamba wa kuku. Ugonjwa huu husambaa kwa kupitia mayai yaliyotagwa na kuku aliyeathirika na ugonjwa huu pia vifaranga walioanguliwa kutokana na mayai hayo huwa na vimelea vya ugonjwa huu.
Vifaranga wanalia kwa kutoa sauti kali
Manyoya yanavurugika
Sehemu ya hajakubwa ya vifaranga hulowana kinyesi
Kuku wakubwa hawaonyeshi dalili zozote.
Kwa vifaranga dalili huonekana kuanzia siku 4 hadi 10, na vifo hutokea baada ya wiki 3 tangu kuanza ugonjwa.
Kuku wanaharisha muharo mweupe.
Teketeza Kuku wote wenye ugonjwa huu
Safisha vifaa vyote bandani kwa kutumia kemikali (Disinfectant) itakayoua vimelea wa magonjwa, pia safisha vifaa vya kuangulia mayai (Incubators).
Nunua kuku au vifaranga wasiokua na magonjwa kutoka kwa wauzaji wanaodhibiti vizuri magonjwa ya kuku
................................................
0 comments:
Post a Comment