Mara
nyingi wafugaji wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika ufugaji wao wa
kuku. Changamoto hizo ni pamoja na wadudu wasumbufu mbalimbali mfano,
Viroboto, Utitiri na chawa. wadudu hawa wamekuwa tishio kubwa katika
kufanya ufugaji wa kuku uwe wenye tija kutokana na kusababisha vifo
vingi.
Katika
banda lako la kuku ukivamiwa na wadudu hawa kwa hakika afya ya kuku
wako itaanza kuzorota kwa haraka na kuwafanya kuku wako waonekane kama
wanaumwa vile. Ni wadudu wanaonyonya damu kwa kiasi kikubwa sana na
hivyo kusababisha kuku kufa kwa ugonjwa wa kuishiwa damu mwilini. Lakini
vilevile kwa kuku wanaotaga huwafanya washushe utagaji wao ghafla.
Ukiwatazama unaweza kuona kama wanaumwa kwa maana wanakonda, kuzubaa na
kupoteza hamu ya kula. Muda mwingi wanakuwa wanajichokonoa na kujikuna
katika manyoya yao kwa kutumia midomo yao. Hii ni kutokana na adha
wanayopata hasa kuwashwa na maumivu wanayosababishiwa.
Viroboto
ni rahisi kuonekana kwa kuwa wanakaa sehemu za wazi za kuku mfano
kuzunguka maeneo ya macho, katika ndevu na mapanga yao nk. Tatizo ni
kwa utitiri na chawa wenyewe si rahisi kuonekana kama mfugaji siyo
mfuatiliaji wa karibu wa kuku wake. Utitiri na chawa wenyewe wanakaa
ndani ya manyoya ya kuku kwenye ngozi kabisa. Utitiri ni mdogo kuliko
chawa. Chawa wanakuwa weupe hivi wanajishika katika ngozi. Utawaona
endapo utapekenyua katika manyoya ya kuku. Wakati utitiri wenyewe
unatakiwa uwe na macho mazuri kuweza kuwaona kwa kuwa ni wadudu wadogo
zaidi lakini ukipekenyua kwenye manyoya na kufika ndani kabisa kwenye
ngozi utawaona wakitembeatembea. Wanapenda kukaa kwenye kwapa za kuku na
kwenye ngozi ya mwili wake
Usipojua vizuri
kuhusu wadudu hawa unaweza ukadhani kuwa kuku wako wanaumwa ugonjwa
mwingine kabisa katika magonjwa ya kuku. Na kwamba utahangaika kutumia
gharama nyingi za madawa huku kuku wako wakiendelea kuzorota bila kupata
nafuu ya matibabu unayohatumia.
Ni muhimu kabla ya kutibu kuku wako ukawasiliana na mtaalamu wa mifugo (Ofisa Ugani)aliye
karibu yako ili aweze kukusaidia kukukagulia na kubaini tatizo halisi
la kuku wako. Kwa maana kuku hawahitaji mchezo wa kubahatisha.
Unatakiwa ujue ni tatizo gani hasa linawakabili kuku wako ili waweze
kupatiwa tiba ya uhakika.
Sasa nini kifanyike kama banda lako litakuwa limevamiwa na Visumbufu hivyo?
Kuna dawa nyingi za kutumia, unaweza kutumia Dawa za unga za kunyunyiza mfano Akheri powder au Sevin (Dudu) Dust.
Dawa hizi utanyunyiza kuku wako wote mmoja baada ya mwengine kwenye
manyoya yao na sehemu zile ambazo zimevamiwa na wadudu hao mfano machoni
na kwenye mapanga yao na vilevile utapaswa dawa hizo kunyunyiza kwenye
maranda au vumbivumbi la ndani ya banda la kuku kwa sababu vumbi ni
makazi mazuri ya Viroboto na Utitiri.
Lakini wakati mwingine unaweza kujitahidi kutumia dawa hizo za kunyunyiza kwenye mabanda na kuku wenyewe lakini zisifue dafu. Mara nyingi nimeliona hili kwenye mabanda mengi ya wafugaji. Sasa ukifikia katika hali hii ufumbuzi wa haraka ni kufanya usafi wa banda lako lote. Ondoa maranda na vumbi lote la samadi kisha deki kwa kutumia dawa ya V- RID Disinfectant.
Pia
utapaswa kupuliza dawa hiyo katika kuta za banda lako. Ukiona tabu
kufanya hivyo basi baada ya kuondolewa samadi yote katika banda lako la
kuku na kufuta vumbi ukutani, deki kwa maji vizuri bila dawa kisha baada
ya banda kukauka vyema paka chokaa kote sakafuni ukutani hadi darini
kama banda lako lina dari na kama halina basi utaishia tu katika kuta za
banda na sakafuni.
Baada ya kukamilisha zoezi hilo ogesha kuku wako wote kwa kutumia dawa ya Paranex, Tik Tik au dawa yoyote ya kuogeshea mifugo
iliyochanganywa
kwenye maji yaliyowekwa kwenye dishi kubwa la lita ishirini au arobaini
au hata ndoo unaweza kitumia. Uogeshaji utafanyika kwa namna ya
kumtumbukiza kuku mmoja mmoja katika lile dishi au ndoo kisha utamtoa.
Ni tendo linalotumia chini ya nusu dakika. Unamtumbikiza unamtoa unamtumbikiza tena unamtoa ni kama mara mbili hivi lengo ni kuhakikisha kuwa dawa inapenya vizuri katika kila sehemu ya mwili wake.
Angalizo.
Unapotumia dawa ya kuogesha ni vizuri zoezi hili likafanyika mchana
wakati jua linawaka ili kusudi kuku waweze kukingwa na athari ya baridi
itakayowasababishia kupata nimonia. Vilevile ni vizuri ukawa na mtaalamu
karibu atakayekusaidia kuchanganya dawa kwa uwiano sahihi na maji ili
kuepusha madhara kama dawa haitachanganywa katika uwiano.
*Kuna baadhi ya vitu uwa
tunawapa kuku kwa mazoea au tunawaachia tu tunapoona wanakula lakini
ukweli vinakuwa na madhara hebu tuviangalie;
vitunguu
vina sumu iitwayo thiosulphate ambayo huua seli hai nyekundu. Iwapo
utalisha kwa kiwango kikubwa itasababisha upungufu wa damu(anaemia) au
kifo.
Maharagwe
mabichi au yasiyopikwa yana sumu iitwayo hemaglutin ambayo ni hatari
kwa kuku kwahiyo unashauriwa kupika au kuchemsha kuondoa sumu hii.
*MCHELE MKAVU.
Kuku wanaolishwa Mchele mkavu kuna hatari mchele huo kujikusanya tumboni na kusababisha matatizo.
*MAGANDA YA PARACHICHI
Kuku
wanapokula maganda ya parachichi itapelekea kuingiza sumu mwilini kwa
hiyo epuka maganda ya parachichi yasije kujichanganya na chakula.
Mbegu za apple zina sumu iitwayo cyanide japokuwa kuku wanapenda apples hakikisha unatoa mbegu.
*VYAKULA VYENYE CHUMVI NYINGI.
Vyakula
vyenye chumvi nyingi husababisha ugonjwa uitwao hypernatremia kwa hiyo
mwili wa kuku hauhitaji kiasi kikubwa cha chumvi. Kuku wanaweza
kuvumilia kiasi kidogo cha chumvi nacho ni 0.25% kwenye maji. Endapo kutakuwa na uhaba inaweza kupelekea ugonjwa huo.
.................................................................................................
.................................................................................................
0 comments:
Post a Comment