Uzalishaji wa maziwa ni biashara nzuri sana na ya kuvutia ambayo huwa na
faida nyingi na humfanya mfugaji kuridhika hasa kwa yule anayependa
kazi hii. Hata hivyo, ni lazima kuanza kwa kuweka msingi imara hata
kabla ya kufikiria ni aina gani ya mbegu utaichukua kwa ajili ya kufuga.
Ni vizuri kufahamu kuwa, usimamizi ni moja ya jambo muhimu sana ambalo
likifanyiwa uzembe linaweza hata kumbadilisha ng’ombe wa maziwa kuwa na
uzalishaji duni kama ngo’mbe wa kienyeji.
Aina mbalimbali za ng’ombe wa maziwa huwa na mahitaji tofauti, hivyo
kiwango cha maandalizi yako ni muhimu sana. Unahitajika kufahamu kuwa,
unalazimika kufikia mahitaji yako kwa ajili ya lishe, si kwenye mahitaji
ya awali tu bali pamoja na mahitaji ya baadaye ya ngo’mbe wako. Suala
hili limefanya wafugaji wengi kushindwa kuendelea kutokana na kuwa
hujiingiza katika shughuli hii bila kuangalia mambo ya msingi
yanayotakiwa pamoja na kuweka mipango thabiti.
Pamoja na kuwa mahitaji yote kwa ajili ya lishe na mambo mengine yako
sawa, ng’ombe wa maziwa ni lazima kuzalisha kulingana na umbile lake na
uwezo wake kamili. Kama utaweza kumudu kufuga ng’ombe halisi wa maziwa,
ni lazima pia utambue kuwa uzalishaji wa juu wa maziwa uhitaji pia
usimamizi wa hali ya juu. Kwa maana hiyo, ni vyema kufuga ng’ombe wa
kiwango cha kawaida (ikiwezekana chotara) ambaye ataendana na uwezo wako
wa kumtunza.
Ni vyema tukaangalia aina mbili za ng’ombe wa maziwa ambao wana uwezo wa kuzalisha maziwa mengi;
(i) Freshiani (Friesian)
Ng’ombe aina ya freshiani ni rahisi kumtambua kutokana na kuwa na rangi
nyeusi na nyeupe, na ni ng’ombe wenye uzalishaji bora wa maziwa. Wanyama
hawa ni wakubwa na pia wanaweza kuwa na mabaka meupe na meusi au
mekundu na meupe. Ikiwa watalishwa vizuri, freshian aliyefikia umri wa
kukomaa huwa na uzito wa hadi kilogramu 550 na urefu wa sentimeta 150
kutoka begani. Mtamba huweza kupandwa, akiwa na umri wa miezi mitano
huku akiwa na uzito wa kilogramu 360.
Wakati baadhi ya ng’ombe wakiwa na uwezo wa kuishi kwa muda mrefu, uwezo
wa kawaida wa kuishi kwa Freshiani ni miaka sita. Hata hivyo, aina hii
ya ng’ombe ni wazalishaji wazuri wa maziwa ambao huweza kuzalisha
kilogramu 7800 kwa wastani kwa muda wa siku 360 yakiwa na kiwango cha
chini cha mafuta ikilinganishwa na aina nyingine ya ng’ombe.
Aidha, aina hii ya ng’ombe huhitaji ulishaji mkubwa hivyo hushauriwa kwa
wafugaji wenye uhakika wa kuwa na lishe bora na ya kutosha kwa mwaka
mzima.
(ii) Ayrshire
Aina hii ng’ombe huwa na miraba ya kahawia na nyeupe karibu sawa na aina
nyingine ya ng’ombe ambao huelekea kuwa na rangi ya (Mahogany). Ng’ombe
hawa huwa na wastani wa kawaida, na uzito wa kilogramu 540 katika umri
wa ukomavu. Aidha, humudu aina yeyote ya ufugaji na si rahisi kupata
matatizo yeyote ya miguu.
Ayrshire huweza kufanya vizuri katika malisho ya aina yeyote tofauti na
aina nyingine ya ng’ombe wa maziwa. Kukiwa na usimamizi mzuri na
ulishaji mzuri, wastani wa uzalishaji wa maziwa ni kilogramu 5400 ikiwa
na kiwango cha juu cha mafuta ukilinganisha na Freshian. Aryshire ni
aina nzuri kwa kufuga hasa kutokana na nguvu aliyonayo pamoja na
uzalishaji mkubwa wa maziwa. Ng’ombe wa aina hii, hutambulika kwa kuwa
na umbo zuri pamoja na chuchu zake kuonekana kuwa zenye ubora. Aidha,
utungaji wa maziwa yake, umefanya maziwa yake kuonekana ni mazuri sana
katika uzalishaji wa siagi na jibini.
Maziwa ya Ayrshire yanafahamika kama “maziwa bora ya kunywa” kutokana na
uwezo wake wa kuwa na mafuta ya kutosha na kiasi kikubwa cha protini.
Kwa mfugaji anayeanza, aina hii ya ng’ombe ni nzuri sana kuanza nayo
kasha baadaye kuongeza freshiani baada ya uwezo wako wa kuhudumia kuwa
imara. Mifugo ya asili ni ghali sana na ni ngumu pia kuwapata, hivyo
basi, njia rahisi kwa wafugaji wa maziwa wanaoanza ni kutafuta ng’ombe
bora wa kawaida ambao mara nyingi huwa ni chotara, kisha kuwaboresha kwa
kutumia mbinu ya kupandikiza dume bora na mwenye uzalishaji mkubwa. Na
hii huhitaji elimu ya kutosha kuhusu uchaguzi wa madume.
*Muhimu: Wakati wa kununua ng’ombe kwa ajili ya kufuga, ni vyema mfugaji
ukatambua kuwa, wazalishaji wa maziwa mara nyingi hawauzi ng’ombe wao
wenye uzalishaji mzuri, badala yake huuza wale ambao hawazalishi kwa
kiwango kizuri, wale wenye matatizo kama kutokushika mimba, wenye
matatizo ya joto na wale ambao hushambuliwa na magonjwa mara kwa mara.
Kwa maana hiyo, pamoja na aina ya ng’ombe unayehitaji kununua, ni muhimu
sana kuwa mwangalifu usije ukanunua ng’ombe mwenye shida yoyote kwani
hapo ndipo mwanzo wa uzalishaji wako kuja kuwa wa matatizo na
kutokufikia lengo.
Kabla mfugaji hajafikiria kuhusu makazi ya ng’ombe wake, ni vyema sana
kujiuliza ni kiasi gani cha mifugo utahitaji kuwa nao baada ya miaka
kadhaa hivyo kukuwezesha kutenga nafasi ya kutosha kwa ajili ya mifugo
utakayoleta.
Njia rahisi ya kulitambua hilo, ni kujiuliza ni kiasi gani cha mifugo
ungependa kuwa nao baadaye na ni kiwango gani cha uzalishaji wa maziwa
ungetarajia kufikisha kutoka kwa ng’ombe wako.
Swali la kwanza, ni muhimu sana kwa mfugaji kujiuliza, kwani kiwango cha
mifugo hutokana na uwezo wa kiwango cha lishe utakachohitajika kulisha
mara kwa mara. Kwa kawaida, ekari moja ya ardhi hutoshea kulisha ng’ombe
wa maziwa aina ya Freshiani mmoja au Jesrey wawili tu.
Ng’ombe wa maziwa mmoja (Fresian, Guernsey, Jersey) kiasi cha tani 5 ya
lishe ya majani mabichi au majani makavu kwa mwaka. Hii ni sawa na
kilogramu 25,000 za matete au kiasi cha majani uliyoyaotesha kwenye
ekari moja. Pamoja na usimamizi mzuri wa malisho ya nyasi, au
mchanganyiko wa malisho kama mikunde au mimea kama desmodium, ni dhahiri
kuwa bado utahitajika kuwa na angalau ekari ya ziada 0.75 ya eneo ili
kuweza kulisha ng’ombe wako vizuri.
Kwa ujumla, ng’ombe wa maziwa huhitaji lishe kiwango kikubwa kuliko
ng’ombe wa nyama, na mara nyingi huwa na uzalishaji mkubwa pale ambapo
ubora wa lishe ni wa hali ya juu. Hali kadhalika, kama utazalisha
malisho yako mwenyewe, bado utahitaji njia nyingine ya ziada ya kupata
lishe ikiwa itatokea tatizo lolote katika malisho.
Jedwahi hili huonesha kiwango cha lishe kinachohitajika kwa aina
mbalimbali ya ng’ombe wa maziwa, pamoja na ardhi kwa ajili ya kuzalishia
malisho.
Ufugaji wa ndani
Katika ufugaji wa ndani, ng’ombe wanahitajika kuwekwa kwenye hali ya
usafi, na makazi yao yawe na ulinzi wa kutosha na yenye kuwapatia uhuru.
Wafugaji walio wengi wamekuwa wakiwekeza fedha nyingi katika kuwajengea
mifugo, na mwishoni kuishia
kukosa fedha kwa ajili ya kulishia mifugo hiyo. Mfugaji anayeanza,
anashauriwa kujengea mifugo yake makazi mazuri na ya gharama nafuu na
baadaye kuendeleza mabanda hayo kutokana na mapato yanayopatikana. Mambo ya kuzingatia katika ujenzi wa mabanda
Nafasi: Ng’ombe mkubwa anahitaji kuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya
chakula, kupumzika pamoja kufanya mazoezi jambo ambalo wafugaji walio
wengi hawazingatii na badala yake huweka mifugo yao katika nafasi ndogo
ambayo mwishoni hudidimiza ukuaji wa mnyama na uzalishaji kwa ujumla.
Kwa mantiki hiyo, ng’ombe mmoja mkubwa anahitaji mita za mraba 8 mbali
na eneo lake la kupumzikia. Njia rahisi ni kutenga eneo hili mbele ya
zizi/banda. Kumbuka, unapokuwa na nafasi kubwa, ndipo unapotengeneza
uzalishaji mzuri.
Paa:
Ni vyema kukawa na paa kwa ajili ya kuilinda mifugo dhidi ya
upepo, mvua pamoja na jua kali. Hakikisha paa linakuwa juu, ili kuipa
uhuru mifugo yako kutembea ndani ya banda bila tatizo lolote. Hakikisha
mteremko wa paa hauwezi kuathiri sehemu ya mifugo kupumzika na sehemu ya
lishe hasa kwa kuruhusu maji kuingia katika sehemu hizo.
Sakafu: Hakikisha sakafu inakuwa na mfumo mzuri wa mifereji kwa
ajili ya kuruhusu maji na mkojo kupita hivyo kuwaweka mifugo katika hali
nzuri. Unaweza kutengeneza sakafu ya simenti ambayo ni rahisi
kusafisha. Hata hivyo kwa kuwa inagharimu fedha, mfugaji anaeanza,
anaweza kutumia udongo wa mfinyanzi au aina nyingine ya udongo mgumu
kutengeneza sakafu. Endapo utasakafu banda, sakafu isiwe inayoteleza kwa
kuwa ng’ombe wanaweza kuteleza na kuumia. Sakafu iwe na mwinuko kidogo
na mwinuko uelekee sehemu ya kutiririshia mkojo na kutolea kinyesi.
Matandiko: Eneo ambalo mifugo hupumzikia, ni vyema kukawa na
matandiko. Unaweza kutumia malighafi ya aina yeyote kavu ambayo huweza
kunyonya mkojo na samadi. Matandiko hayo ni lazima kubadilishwa mara kwa
mara.
Vihondi vya maji na chakula: Hakikisha kuna vihondi vya kutosha
kwa ajili ya chakula na maji. Mabanda ni vyema yakawa karibu na vyanzo
vya upatikanaji wa maji safi na salama. Kwa wastani, ng’ombe mmoja
anahitaji kunywa maji kiasi cha lita kati ya 50 au 80 kwa siku sawa na
ndoo 5 hadi 8 za maji (za ujazo wa lita 10).
Shimo la mbolea: Mifugo inayolishwa vizuri hutoa samadi nyingi
hivyo huweza kuwa tatizo kwa watu wanaokuzunguka hasa ikiwa inatapakaa
kila mahali na kusababisha kuwepo kwa harufu mbaya. Kama utafuga mifugo
mingi katika eneo dogo bila kuwa na sehemu maalumu ya kuweka mbolea
inayotokana na mifugo hiyo, basi ni dhahiri kuwa utasababisha
kutokuelewana na majirani, lakini pia kutasababishia wanyama kukaa
katika hali ya usumbufu. Ni vyema kuandaa shimo maalumu kwa ajili ya
samadi hasa kwa ufugaji wa ndani, kabla ya kutumia kwa ajili ya kuweka
kwenye mashamba ya malisho.
Namna ya kuanza ufugaji kwa urahisi
Kabla ya kuamua kufanya biashara ya uzalishaji wa maziwa, maandalizi
mazuri ni moja ya sababu itakayokupa mwanga kufanikiwa au
kutokufanikiwa. Hata kabla ya kuwaza nia aina gani ya ng’ombe utanunua,
ni lazima kufikiri kwanza ng’ombe huyo utamlisha nini.
Fikiria lishe, fikiria nyasi
Ili kufuga ng’ombe, ni lazima uwe na lishe ya kutosha. Huwezi
kumuendeleza ng’ombe kuzalisha wakati hauna lishe bora ya kutosha, ikiwa
ni pamoja na nyasi, mikunde na majani ya nafaka. Moja ya njia nzuri ya
kuzingatia ni nyasi. Mfugaji anayeanza, ni lazima kuzingatia haya kwa
ajili ya lishe;
Hakikisha unatunza nyasi za asili zilizopo katika shamba lako la malisho
Ongeza kwa kuotesha majani mengine mapya katika shamba lako
Nunua malisho ambapo unaweza kuswaga mifugo yako kwenda kula
Kodisha au nunua eneo kwa ajili ya kuotesha malisho kisha kukata na kupeleka kulishia mifugo
Nunua majani kutoka kwa watu wanye malisho au wanaofanya bishara ya kuuza majani yaliyokatwa tayari ...............................................................
0 comments:
Post a Comment